Sababu 5 kwanini Vijana wajitokeze kwa wingi zaidi uchaguzi 2020?

Mwaka 2020 ni mwaka wa uchaguzi mkuu nchini Tanzania, hivyo ifikapo mwezi Oktoba raia wote waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura watapata nafasi ya kuchagua viongozi wanaoamini watasimamia serikali kwa misingi ya utawala bora. Hata hivyo vijana wapo hatarini kutojitokeza kushirki katikai zoezi hili kwa ukamilifu. Hii inatokana na kwamba vijana wengi hawana elimu na msukumo wa kutosha kuhusu masuala ya kiraia. Hivyo basi jitihada za ziada zinaitajika kuwafikia vijana kwa kutengeneza ujumbe ambao unaweza kuwafikia kwa wakati kabla ya zoezi la kupiga kura. Hata Hivyo vijana weneyewe inabidi tutambue thamani ya mchango wetu katika kulijenga taifa

Hizi ni sababu 5 kwanini ni muhimu vijana wa kitanzania wasiipoteze haki yao hii ya msingi.

  1. Vijana ni nusu ya wapiga kura wote na hivyo wana nguvu kubwa ya kuhamasisha viongozi watakao chaguliwa Kwamijibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 vijana wenye umri wa miaka 15-35 ni takriban 35.1% ya watanzania wote. Hii inamaanisha ya kwamba vijana wanauwezo mkubwa wa kushawishi na kuamua ni kiongozi wa aina gani achukue madaraka. Katika utafiti uliofanywa na shirika la maendeleo linaloongozwa na vijana la Restless Development ni 61% pekee ya vijana walio na umri kati ya miaka 18-29 walisema watajitokeza kupiga kura.  Ni muhimu kutambua kuwa umoja wetu ndio nguvu yetu, kwa mmoja mmoja ni rahisi kuamini kuwa kura yako haina nguvu, lakini kwa umoja wetu tunaweza kumchagua kiongozi mwenye kutetea maslahi yetu.
  2. Vijana ni moja ya wahanga wa sera na mikakati ya serikali yao Kisingizio kikubwa kwetu vijana katika ushiriki wa shughuli za kiuchaguzi ni kwamba muda wetu bado haujafika. Jambo la muhimu kukumbuka ni kwamba ndani ya miaka minne, ambayo haukufanya maamuzi maisha yako yatabadilika sana. Mwanafunzi wa chuo ataanza kutafuta kazi, wakati takwimu zilizotolewa na shirika la  “United States Agency for International Development (USAID) KATIKA REPOTI YA PROGRAM YA “Feed the Future” ya mwaka 2016-2017 takriban vijana 800,000 wapya wanaingia katika soko la ajira kila mwaka. Wakati ripoti ya International Development Research Centre ya mwaka 2015 ineleza kwamba inamchukua kijana aliyemaliza chuo kikuu wastani wa miaka 5.5 kupata ajira. Wakati huohuo kuna vijana watakaojiunga na masomo ya elimu ya juu na kuhitaji mikopo wakati kwa mwaka huu ni wanafunzi 30,675 kati ya 87,000 waliiomba mkopo. Vilevile wapo vijana watakao jiajiri na kuanza biashara zao huku masharti ya mikopo yaki mkandamiza mfanyabiashara mchanga. Hivyo basi ni wazi kwamba sera na mifumo ya elimu,ajira na kodi itaanza kuwaathiri moja kwa moja.
  3. Vijana wanayo nafasi kubwa zaidi ya kuwafahamu wagombea katika kizazi hiki cha mitandao ya jamii Moja wapo ya faida kubwa ya kuzaliwa katika nyakati hizi za utandawazi ni urahisi wa upatikanaji ya habari na taarifa muhimu. Kwa mujibu wa wavuti ya uchambuzi wa trafiki za kimtandao wa statcounter tovuti vijana wenye umri kati ya miaka 18-35 tunaongoza kwa kutumia mitandao ya kijamii nchini ambapo ni takriban 75% ya watanzania wenye ujuzi wa kutumia mitandao ya jamii na pia ndio wenye atumizi ya mara kwa mara. Elimu ya mpiga kura inaweza kumfikia kijana kwa urahisi zaidi kupitia Facebook, Twitter, Youtube na instagram kuliko magari ya matangazo. Hii inamaanisha kuwa habari zinaweza kupatikana kwa haraka zaidi  na hivyo kuwapa vijana nafasi sio tu ya kupiga kura lakini pia kuwa wapiga kura wenye upeo na ufahamu mzuri wa wasifu wa wagombea wao na haki zake.
  4. Vijana pekee ndio tunaweza kuhakikisha vijana wenzatu wanapata madalaka serikalini Sio rahisi kwa mgombea kijana kupita kama mgombea, kwanza ndani ya chama chake cha siasa na pili katika uchaguzi mkuu. Jamii yetu haina utamaduni wa kurithisha madakaka kwa vijana na kuwaamini katika nafasi za uongozi, hii inatokana na imani kwamba watuwazima ndio wenye jukumu na busara za kuonngoza na kutoa maamuzi. Bunge letu la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania lina takriban wabunge vijana 47 kati ya wabunge 393 .Jambo la kushtusha ukizingatia kwamba kwa mujibu ya tovuti ya IndexMundi taifa letu lina wastani wa umri wa miaka 17.9 . Uwakilishi mdogo wa vijana unadhoofisha nguvu ya ajenda ya vijana na mabadiliko katika sera na sheria zinazowaguza vijana.
  5. Ni muhimu kwa vijana kujijengea utamaduni wa kushiriki shughuli za kiraia mapema Vijana ndio nguvu kazi na taifa la leo, na endapo hatutajali mifumo ya siasa na shughuli za kiraia taifa letu linaelekea mahala pabaya. Nchi nyingi duniani zimeanza taratibu za kushusha umri wa kikatiba wa kupiga kura ilikuwahusisha vijana kuanzia miaka 16. Mfano mzuri ni nchi ya Scotland Uingereza ambapo vijana wa umri wa miaka 16 na 17 wanaweza kushiriki kuchagua wabunge na viongozi wa serikali za mitaa. Nchi ya Nigeria pia imekuwa mfano wa kuigwa baada ya kupitisha sheria ya “Not Too Young to Run” ya mwaka 2018 ambayo ni kupunguza umri wa kugombea nafasi za uteuzi wa Baraza la Mkutano na Baraza la Wawakilishi kutoka umri wa miaka 30 hadi 25, Seneti na Utawala kutoka umri wa miaka 35 hadi 30 na ofisi ya rais kutoka 40 hadi 30 na mgombea wa uhuru nchini Nigeria.

Hivyo basi ni muhimu kuzingatia ya kwamba mabadiliko hayajawahi kutokea kwa kutopiga kura na kuwaachiwa wengine wafanye  maamuzi makubwa ya kisiasa. Ili vijana tuweze kuhamasisha mabadiliko tunahitaji tunatakiwa kuwanyanyua wagombea wanaoyesha nia ya dhati katika kutatua matatizo ya vijana ikiwemo wagombea vijana wenyewe. Hakuna mtu mwingine atakayepiga kura kwa maslahi ya vijana isipokuwa vijana.en_USEnglish
swSwahili en_USEnglish