Kwanini vijana hawajitokezi kupiga kura?

Vijana wamekuwa mstari wa mwisho katika kushiriki kwenye shughuli za kiraia hasa katika zoezi zima la upigaji kura. Wakati huo huo tunatambua kwamba ili kuleta maendeleo raia wanajukumu la kulinda maadili ya umma na kufanya mabadiliko muhimu katika jamii na kwa taifa zima. Kunapokuwa na mtengano katika ushiriki wa shughuli za kiraia kwa kundi kubwa katika jamii hasa katika upigaji kura, kunakuwa na mapungufu makubwa katika uwakilishi wa makundi hayo. Jambo hili linalopelekea kutokuwa na usawa katika utekelezaji wa mahitaji yao serikalini. Kwa kuzingatia hali hii ni muhimu kujua vyanzo vinavyosababisha vijana kuwa nyuma sana katika kutumia haki  ya kushiriki katika shughuli za kimaamuzi.

Ukosefu wa maarifa ya kisiasa na uraia

Vijana wanao ufahamu mdogo sana juu ya haki zao na taratibu za shughuli za kimaamuzi. Idara na mashirika ya serikali hazijatoa msaada wakutosha wa kujenga kampeni za media zinazozungumza lugha ya vijana ili kukuza umuhimu wa ushiriki. Katika utafiti uliofanywa na shirika la maendeleo linaloongozwa na vijana la Restless Development ni 61% pekee ya vijana walio na umri kati ya miaka 18-29 walisema watajitokeza kupiga kura. Vyama vya siasa na viongozi waliochaguliwa pia wamekuwa na juhudi ndogo katika kuwashirikisha vijana katika mijadala inayolenga agenda mbalimbali za vijana. Wakati huo huo vijana hawanamuako wa kujiunga na vyama vya siasa hivyo wanashindwa kushiriki kikamirifu na kuvielewa vyama kwaundani.

Ukosefu wa uaminifu na ujasiri wa kushiriki

Inadaiwa kuwa vijana hawapendi siasa na serikali, hii yote ni kwa sababu hawana imani na wanasiasa na mifumo ya kisiasa, na hawaamini kuwa kura zao zitaleta tofauti. Ukosefu wa hamasa pia unasababisha vijana kuona serikali haielewi mahitaji na maslahi ya yao. Vijana wachache ambao wamejiunga na vyama siasa hawapewi kipaumbele katika kuandaa ilani za vyama na kushikiria nafasi za uongozi na badala yake wanatumika kama askari wa miguu wa wagombea wakubwa na kufanya kampeni za hamasa za kutafuta wanachama wapya. 

“Kwa mujibu wa wavuti ya uchambuzi wa trafiki za kimtandao wa “statcounter” tovuti vijana wenye umri kati ya miaka 18-35 tunaongoza kwa kutumia mitandao ya kijamii nchini ambapo ni takriban 75% ya watanzania wenye ujuzi wa kutumia mitandao ya jamii.”

Umbali kati ya serikali na vijana

Utandawazi pia umeongeza pengo kati ya vijana na taasisi za kisiasa, na kuathiri vibaya upigaji kura. Katika ulimwengu wa media nyingi kuliko maelezo, ambapo habari imeenea sana, vijana wengi wanakuwa “wakipata mafuriko ya taarifa za uongo na ukweli pasipo na uwezo wa kuzichanganua na kupata nafasi ya kujibiwa maswali yao”. Hali hii ya kuwa na maswali mengi pasipo na majibu ya kutosha hutengeneza hali ya wasiwasi  na kusababisha vijana kuhisi kuna maswala mengi ya kushughulikia na hakuna la maana linalotendeka kwaajili yao.

Hatua ya mpito ya maisha

Ni vigumu sana kwa vijana wadogo kati ya miaka 18 na 24 kuona thamani ya kushiriki katika shughuli za kiraia. Hii ni kwa sabubu muda wao mwingi wanatafuta kazi za kuwaletea kipato,wapo masomoni, wanajiandaa kuhama nyumba za wazazi wao kwenda kujitegemea na kadhalika. Wakati huu vijana wanajali zaidi namna vijana wenzao wanavyowachukulia, na kufuata makundi wakitafuta muelekeo wa maisha. Shughuli za kisiasa na upigaji kura wala hazipo katika orodha ya mahitaji yenye kipaumbele.

Tunafanya nini sasa kuwafikia vijana? Ili kufikia ushiriki mkubwa wa vijana tunahitaji kutengeneza mazingira yanayoleta ushawishi wa vijana kushiriki katika uchaguzi. Vijana huelewa zaidi kwa lugha ya burudani, hivyo matamasha, sanaa na muziki ni rahisi kuwafikishia ujumbe. Uwepo wa mijadala ya mara kwa mara ya matatizo yanayo wakabili vijana kunaweza pia kuwavutia vijana kusikiliza sera za wagombea na hatimaye kushiriki katika kupiga kura. Hivyo basi ikiwa tunataka kubadili athari za kitaifa na kuunda demokrasia shirikishi ambayo upigaji kura ni tabia iliyoenea kwa vijana hatuna budi kuzungumza na vijana kwa lugha yao.en_USEnglish
swSwahili en_USEnglish